Fungua macho yako na uchukue kila hatua kwa dhati.
Fungua macho yako ya ndani katika jiji hili zuri la moyo, tazama huku na huku
na uone barabara hizi nzuri. Uone amani ikija kukuelekea. Kisha simama
tuli. Simama tuli kabisa, kabisa, ili amani iweze kukupata. Usisogee.
Usisogee.
Iache ije, ikuguse, ikuzunguke kabisa.
Uache upendo huo mzuri ulio ndani yako uje na kukukumbatia. Simama tuli.
Tuli kabisa, kabisa.
Si kwa kujificha kwenye kona fulani ya wazo fulani, au ndoto fulani.
Bali simama katika barabara pana zaidi, katikati ya makutano yenye shughuli nyingi zaidi.
Ni wakati wa kuwa dhahiri.
Usijifiche kana kwamba umetoweka.
Huu si wakati wa kufanya hivyo katika maisha yako — kila siku uliyopewa
ni siku ambayo unaweza kutembelea jiji la moyo. Na huu si wakati wa
kujifanya "mnyenyekevu" — hapana. Ni wakati wa kujidhihirisha wazi.
Kama vile uhai huu ulivyo dhahiri. Kama vile pumzi hii ilivyo dhahiri —
sivyo? Dhahiri kabisa.
Kuwepo kwako ni dhahiri; hakujifichi chini ya mwamba fulani mlimani.
Hakujifichi chini ya majani katika msitu fulani wenye kijani kibichi.
Hapa, kila kitu kiko wazi. Shauku yako ya ndani iko wazi.
Imekuwapo daima, nayo inatamani kutimizwa.
Na maajabu ya maajabu, muujiza wa miujiza umetokea — umepewa uhai.
Umepewa maisha ili jambo hili liweze kutokea. Ili jambo hili liweze kujidhihirisha.
Kuwepo huku ni nini? Usikidharau.
Kuwepo huku ni nini? Nitakuambia kuwepo huku ni nini.
Ni jambo la pekee sana. Na unajua kwa nini ni la pekee?
Kwa sababu ni daraja; ni daraja la ajabu kati ya kilicho na ukomo na kisicho na ukomo.
Hapa ndipo jambo hili hutokea. Hapa ndipo vitu hivyo viwili hukutana.
Hiki ndicho kizingiti ambacho vitu hivyo viwili vinaweza kukutana — ambapo mwanadamu mwenye kufa anaweza kupata uzoefu wa kutokufa.
Fursa kuu kuliko zote.